
Chama kikuu cha upinzani cha Congress nchini India kimeitisha mgomo katika jimbo la Chhattisgarh ambako wanawake 13 wamepoteza maisha kutokana njia za uzazi wa mpango zinazotolewa kwa njia ya upasuaji.
Wanawake sitini wako hospitalini kati yao 20 wako kwenye hali mbaya baada ya upasuaji huo.
Jopo la madaktari kutoka mjini Delhi wamefika katika jimbo hilo kusaidia hali hiyo ya dharula.
Serikali ya Chhattisgarh imetoa amri kufanyika uchunguzi kuhusu vifo vilivyojitokeza, huku waziri Kiongozi, Raman Singh akisema kuwa tukio hilo limetokea kutokana na uzembe wa madaktari.
Familia za waathirika, wote kutoka familia masikini zimeahidiwa kulipwa fidia ya takriban dola za marekani 6,600.
Maafisa wa afya wanne wamesimamishwa kazi na madai dhidi ya Daktari aliyefanya upasuaji yameshafikishwa Polisi.
Lakini chama cha Congress kimefanya maandamano kushinikiza Waziri wa afya Amar Agrawal kujiuzulu.
Namna ambavyo upasuaji huu hufanyika:
upasuaji huu hufanyika kwa kuziba mirija ya uzazi ambayo hubeba mayai kutoka kwenye Ovari kwenda tumboni, hubanwa kwa kutumia vitu mfano wa vibanio au pete ndogondogo au kwa kukata mrija.Hatua hii huzuia mayai na mbegu za kiume kukutana, hivyo mimba haiwezi kutungwa.
Mayai nayo kutoka kwenye ovari kama kawaida, lakini badala yake yatapotelea mwilini.

Njia hii huwa ya mafanikio ikiwa itafanyika inavyopaswa na mtaalam wa hali ya juu, hata hivyo kuna madhara ambayo huweza kujitokeza.
Madhara
Kuna hatari ya kuharibika kwa ogani nyingine wakati wa operesheni . Damu huweza kutoka kwa wingi pia maambukizi, pia njia hii ya uzazi wa mpango ni ya kudumu , hali haiwezi kurejea tena kama awali kama inavyokua kwa njia nyingine za uzazi wa mpango.
Mamlaka nchini India imekua ikipigia upatu sana swala la uzazi wa mpango kwa miongo kadhaa kwa ajili ya kuwashawishi watu kuwa na familia ndogo.