Msanii wa muziki wa hip hop
nchini, Rashid Makwaro ‘Chid Benz’ jana alizuiwa na askari kuingia ndani
ya chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa
sababu ya mavazi na mapambo yake mwilini.
Chid Benz alifika mahakamani hapo kusikiliza kesi
yake lakini kutokana na mavazi aliyovaa, mapambo na kipini puani
alijikuta akizuiwa. Aliwasili mahakamani hapo asubuhi ili kusikiliza
kesi yake inayomkabili ya kukutwa na dawa za kulevya iliyokuwa itajwe
mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema. Lakini, wakati akitaka kuingia
ndani ya chumba cha mahakama, askari aliyekuwa mlangoni alimtaka
apandishe suruali yake aliyokuwa ameivaa mtindo wa mlegezo na afunge
vishikizo vya shati lake ili kuificha cheni ya kiasili aliyokuwa ameivaa
shingoni.
Mbali na hayo, askari huyo alimtaka Chid Benz pia
avue miwani aliyokuwa ameiva na kipini kilichokuwa kikining’inia puani
na baada ya kukamilisha utaratibu huo aliruhusiwa kuingia mahakamani kwa
ajili ya kuendelea kusikiliza kesi yake.
Baada ya msanii huyo kuingia mahakamani, mawakili
wa Serikali, Ofmed Mtenga na Leonard Challo waliomba kesi hiyo
iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika, wakiomba
ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa. Hakimu Lema alikubaliana na maelezo
hayo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Desemba Mosi kwa ajili ya kuangalia
kama upelelezi wake utakuwa umekamilika au la.
Awali, Chid Benz alitishia kuwapiga wapigapicha
huku akitoa maneno makali dhidi yao, lakini mama yake aliwaomba
wasimpige picha kijana mwenzao, lakini askari walimweleza mama huyo kuwa
waandishi hao wapo kazini, waachwe wafanye kazi yao.